Kwa mujibu wa Kitengo cha tarjama cha Shirika la Habari la Hawza, Ufaransa itashuhudia wimbi jingine la maandamano ya nchi nzima siku ya Jumamosi, tarehe 14 Novemba. Wanaharakati wa vuguvugu la Mavazi ya Njano pamoja na mashirika ya vijana, makundi yanayotetea haki za watoto na wale wanaopinga vitendo vya ukatili wa polisi wanatarajiwa kujitokeza mitaani.
Kwa mujibu wa taarifa ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Ufaransa, maandamano kati ya 50 na 60 yanatarajiwa kufanyika katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo.
Katika maandamano ya wiki iliyopita, idadi ya washiriki ilifikia watu 146,000 kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya Mambo ya Ndani, huku Muungano wa Mashirika ya Vijana ukikadiria kuwa idadi hiyo ilikuwa watu 250,000.
Makundi mengine pia yatajiunga na mikusanyiko hiyo yakiwa na madai mbalimbali, yakiwemo kupinga ukatili dhidi ya watoto na vijana, kupinga rasimu ya sheria inayopendekeza kuwepo kwa dhana ya uhalali wa matumizi ya silaha na askari polisi, kutetea mustakabali wa watoto na kulinda mazingira.
Katika mji wa Paris, maandamano ya pamoja yataanzia katika Uwanja wa Jamhuri (Place de la République), kisha kupita eneo la Bastille na kuelekea katika Uwanja wa Nation. Njia hiyo imeidhinishwa na Ofisi ya Mkuu wa Polisi wa Mkoa.
Vyama vya wafanyakazi, vikiwemo CGT, FSU na FO, pia vimeshiriki katika uratibu wa maandamano hayo.
Wakati huohuo, Laurent Nuñez, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Ufaransa, ametangaza kuwa takribani askari polisi na wanajeshi wa kikosi cha Gendarmerie 70,000 watawekwa katika hali ya tahadhari na kupelekwa kazini kwa ajili ya kuhakikisha usalama wakati wa maandamano hayo. Ameeleza kuwa hatua za kiusalama zinazofanana na zile zilizochukuliwa katika wiki zilizopita zitatekelezwa.
Akizungumzia uwezekano wa kutokea mvutano na matukio ya hapa na pale wakati wa maandamano hayo, waziri huyo amewaomba wakuu wa mikoa kuchukua hatua zinazohitajika kwa ajili ya kusimamia na kudhibiti mikusanyiko hiyo.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa askari polisi kuzingatia mifumo na taratibu za kisheria wanapotumia vifaa vya kudhibiti mikusanyiko, vikiwemo mabomu ya kurushwa kwa mkono (grenades).
Pia amesisitiza umuhimu wa kuhakikisha usalama na ulinzi wa waandishi wa habari, kuheshimu haki zao na kuwawezesha kutekeleza majukumu yao ya kuripoti na kuhabarisha umma kuhusu maandamano hayo.
Maoni yako